Bodi inayosimamia ligi kuu Uingereza imetangaza rasmi tarehe 1-Septemba kama tarehe ya kufungwa kwa dirisha la usajili kwa msimu unaokuja wa 2020-2021.
Uamuzi huo umefanyika mara baada ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo kukaa chini na kupiga kura kwamba tarehe ya kufungwa kwa dirisha hilo kubwa kwa msimu unaokuja lifungwe siku hiyo ya tarehe 1-Septemba badala ya uamuzi uliofanyika mwanzo ambapo dirisha la usajili la msimu huu lilifungwa tarehe 8-Agosti.
Uamuzi huo umefikiwa mara baada ya klabu za ligi kuu Uingereza kuonekana zinashindwa kuendana sawa na ubora wa kikosi haswa kutokana na msimu huu dirisha la ligi kuu Uingereza kufungwa kabla ya madirisha mengine ya ligi nyengine barani Ulaya kufungwa.
Kwa kawaida kabla ya msimu huu madirisha yote ya ligi barani Ulaya yalikuwa yanafungwa siku moja kabla ya ligi kuu Uingereza kufikia makubaliano kwamba msimu huu dirisha la usajili litafungwa kabla ligi haijanza wakati hapo kabla ilikuwa ligi inaanza kisha dirisha linafungwa sawa na madirisha mengine ya ligi barani Ulaya wakati michezo kadhaa ya msimu mpya imeshachezeka.
Kanuni na taratibu zilivyo ni kwamba kama dirisha la usajili kwenye ligi yako likiwa limefungwa klabu yako haitotakiwa kusajili mchezaji lakini itakuwa inaruhusiwa kuuza na hilo lilionekana lina madhara kwa timu za ligi kuu Uingereza ambazo dirisha lake likiwa limefungwa na madirisha ya ligi nyengine yakiwa hayajafungwa basi timu za ligi nyengine zingeruhusiwa kusajili wachezaji kutoka Uingereza bila timu zenyewe kuziba mapengo ya wachezaji walioondoka.
No comments:
Post a Comment