Fabregas aibuka shujaa, Chelsea ikiondoka na ushindi Liberty Stadium - Darajani 1905

Fabregas aibuka shujaa, Chelsea ikiondoka na ushindi Liberty Stadium

Share This

Cesc Fabregas anaibuka shujaa kwenye mchezo wa leo mara baada ya kuifungia Chelsea goli pekee na la ushindi na kuifanya Chelsea iondoke na alama zote tatu kwenye uwanja wa Liberty ambapo Chelsea imeitandika Swansea goli 1-0.

Alipokea pasi nzuri kutoka kwa Eden Hazard na kutotaka kufanya hajizi akionganisha kwa mguu wake wa kushoto na kuipatia Chelsea goli hilo la ushindi mnamo dakika ya 4 ya kipindi cha kwanza.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilitawaliwa na pande zote mbili ambapo Swansea iliyokuwa nyumbani ilijitahidi kupambana ili kutafuta matokeo chanya ili iweze kujinasua na hatari ya kushuka daraja, wakati Chelsea ilitambia goli lake la mapema lililowafanya kucheza mpira kwa kujiamini huku ikitengeneza mashambulizi haswa kupitia pembeni lakini pia ikimtumia zaidi nyota wake Eden Hazard ambaye ufundi wake wa kumiliki mpira kwa muda mrefu ukiongeza na ujuzi wa Cesc Fabregas wa kupiga pasi zilizoshiba ukisaidia kwa ukubwa kwenye safu ya mashambulizi.

Kipindi cha pili kilikuwa kizuri, haswa kwa Swansea walioonekana kutafuta ushindi zaidi huku ikiwatumia wachezaji wake mashuhuri lakini ukuta wa Chelsea ulioongozwa na nahodha wake Gary Cahill ulionyesha kudhibiti kwa kiasi kikubwa mashambulizi hayo lakini pia N'Golo Kante akionyesha kufanya kazi kubwa huku Tiemoue Bakayoko akionekana kuanza kuuzoea mchezo na aina ya mpira wa Uingereza.

Mabadiliko yaliyofanyika leo katika safu ya ushambuliaji ukilinganisha na mchezo uliopita katika kikosi cha Chelsea ni kutokana na mfumo ambapo mchezo uliopita Chelsea ilitumia mfumo wa 3-4-3 huku ikiwa na washambuliaji watatu ambao ni Eden Hazard, Olivier Giroud na Willian wakati leo imeanza kwa kutumia mfumo wa 3-5-2 ambapo katika safu ya ushambuliaji iliongozwa na Hazard na Olivier Giroud ingawa baadae kocha Antonio Conte alibadili mfumo na kutumia 3-4-3 kwa kuwatoa Hazard na Giroud ambao nafasi zao zilichukuliwa na Willian na Morata wakati kwa upande wa Fabregas aliyekuwa akicheza kama kiungo nafasi yake ilichukuliwa na Pedro aliyeingia na kucheza kama mshambuliaji katika mfumo wa washambuliaji watatu.

Kwa matokeo haya, Chelsea inakuwa imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kupambania nafasi ya kucheza klabu bingwa Ulaya msimu ujao ambapo kwa sasa imebakiza pengo la alama mbili dhidi ya Tottenham inayoshika nafasi ya nne huku hapo kesho ikiwa na mchezo mgumu dhidi ya klabu kutoka jiji moja, jiji la London, klabu ya Watford.

No comments:

Post a Comment