Wakongwe wa Chelsea wapambana na wa Inter Milan, hongereni kwao - Darajani 1905

Wakongwe wa Chelsea wapambana na wa Inter Milan, hongereni kwao

Share This

Lilikua ni jambo la kufurahisha lililorudisha hisia za mbali kwa kila mchezaji na shabiki kwenye uwanja ule wa Stamford Bridge mara baada ya magwiji wao kurejea uwanjani, sio kurejea tu ili kutoa heshima ila kutoa heshima kwa kuwakumbusha soka safi walilolipiga na kulicheza kwa miaka hiyo.

Ni mchezo wa wakongwe wa Chelsea ambao waliohusika ni wale wachezaji waliowai kupita klabuni hapo ambao walijiunga kwa pamoja na kuunda timu ya Chelsea Legends huku wakicheza dhidi ya wakongwe wa Inter Milan waliojiita Inter Forever.

Mchezo huo ulianza kwa kutoa heshima kwa gwiji wa Chelsea, Ray Wilkins ambaye alifariki mwaka huu na ndipo mchezo ukaanza ambapo timu ya Chelsea Legends iliundwa na nyota wengi wa zamani kama Gianfranco Zola, Roberto di Matteo, Michael Essien, Dennis Wise, Andrey Shevchenko, Michael Ballack, Gianluca Vialli ambaye huyu alipita Chelsea akiwa kama kocha mchezaji na wachezaji wengi bila kumsahau na Carlo Cudicini ambaye ndiye kocha wa makipa klabuni Chelsea aliyechaguliwa kuwa nyota wa mchezo lakini pia Marcel Desailly, na nyota wengine kibao.

Mchezo ukachezwa na goli la Chelsea lilikua ndilo goli la kwanza katika mchezo huo lilifungwa na aliyewai kuifundisha Chelsea na kuipa taji la klabu bingwa Ulaya, Roberto di Matteo ambaye alipiga shuti la mbali na kumfanya mlinda mlango wa wapinzani kuishia kugaragara. Uwezo bado haujaisha. Kilichoisha kwa gwiji huyu ni nywele kichwani maana kwa shuti alilopiga ni kama alivyokua klabuni hapa huku akiwa kijana. Hatimaye mchezo ukaisha kwa Chelsea Legends kupoteza kwa magoli 1-4.

Mara baada ya mchezo kuisha kulifanyika matukio mengi ambapo mojawapo ni pale wakongwe hao walipozunguka uwanja na kutoa shukrani kwa mashabiki.

Mchezo huu pia ulikuwa maalumu katika kukusanya pesa kwa kuchangia taasisi ya Chelsea, Chelsea Foundation ambayo hutumia michango hiyo iliyopatikana kwenye ukusanyaji wa viingilio na kuvitumia kwenye utunzaji wa jamii.

No comments:

Post a Comment