Ufafanuzi kuhusu michuano mipya ya UEFA - Darajani 1905

Ufafanuzi kuhusu michuano mipya ya UEFA

Share This
Nilikuletea taarifa kuhusu chama cha soka barani Ulaya maarufu kama UEFA kuthibitishisha juu ya michuano mipya ambayo imeanzishwa na chama hicho kwa ajili ya klabu za barani humo.


Lakini mara baada ya kutoka kwa taarifa hiyo nimepokea maswali kadhaa kutoka kwa mashabiki wa soka na wapenzi wa mchezo huo juu ya ufafanuzi zaidi kuhusu michuano hiyo.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza msimu wa 2021-2022 ikishirikisha klabu 32 na itakuwa katika mtindo wa makundi ambapo pia kuanzishwa kwa michuano hii kutamaanisha klabu zinazoshiriki michuano ya ligi ya Ulaya yaani Europa League kupungua kutoka timu 48 mpaka klabu 32 ambazo zitaunda makundi nane sawa na michuano ya klabu bingwa barani Ulaya (UEFA Champions League)

Lakini pia kuanzishwa kwa michuano hii kutamaanisha klabu zinazoshiriki michuano ya Ulaya kuongezeka kutoka klabu 80 mpaka kufikia klabu 96 ambapo klabu 32 zitakuwa za Klabu bingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League, klabu 32 zitashiriki Ligi ya Ulaya maarufu kama Europa League na klabu 32 zitashiriki michuano hiyo mipya.

Hayo ndiyo machache unayopaswa kuyajua kuhusu michuano hiyo. Lakini kuhusu mfumo wa uchezaji itakuwaje hiyo bado haijafafanuliwa na chama hicho cha soka kutoka barani Ulaya ambapo wamesema wanaendelea kufanya mazungumzo ili kuona wataiendesha kwa mtindo wa aina gani.

Moja ya sababu ambayo naiona imefanya kuundwa kwa michuano hii ni ili kuzidi kuongeza wawekezaji na udhamini na kuzidi kuzivutia chaneli za televisheni kuzidi kuwekeza katika soka la barani Ulaya. Ni kama walivyoeleza sababu ya kuamua kuanzisha michuano ya ligi ya timu za taifa (UEFA Nations League) ambapo walisema wameamua kuianzisha ligi hiyo ya timu za taifa ili kuzidisha thamani ya michezo hiyo na kuitoa katika mtindo wa michezo ya kirafiki. Kwa hivyo kubwa walilolinlenga katika michuano hii ni sababu za kibiashara na udhamini.

No comments:

Post a Comment