Chelsea yaingia matatani kuuzwa uwanja wa Wembley - Darajani 1905

Chelsea yaingia matatani kuuzwa uwanja wa Wembley

Share This

Moja kati ya taarifa kubwa zilizosambaa na kutikisa vyombo vingi vya habari hapo jana haswa huko nchini Uingereza ni juu ya taarifa kuhusu mmiliki wa klabu ya Fulham, Shahid Khan kupeleka ombi kwenye chama cha soka nchini Uingereza, FA juu ya kuununua uwanja wa taifa wa nchini humo maarufu kama Wembley.

Mmiliki huyo mwenye asili ya bara la Asia anatajwa kuwa tayari kutoa kiasi cha paundi milioni 800 ambapo inaweza pia kufikia paundi bilioni 1 ili kuununua uwanja huo unaopatikana kwenye jiji la London nchini Uingereza. Jiji hilo pia kunapatikana klabu kama Tottenham ambayo kwa sasa inautumia uwanja huo kama uwanja wake wa nyumbani kutokana na uwanja wake wa White Hart Lane kuwa kwenye matengenezo, Arsenal, West Ham na hata Chelsea.

Kuuzwa kwa uwanja huo kunaweza kuwa habari mbaya kwa klabu za London ambazo zimekuwa zikiutumia uwanja huo kama uwanja wa dharura, lakini inaweza ikaleta madhara makubwa na ikawa ni habari mbaya kwa Chelsea kutokana na mipango yake ya kuupanua uwanja wake wa Stamford Bridge huku ikilenga kuutumia uwanja wa Wembley kwa dharura wakati uwanja wake ukiwa kwenye matengenezo.

Chelsea imekuwa na mpango wa kutumia paundi bilioni 1 ili kuupanua uwanja wa Stamford Bridge huku ikiapanga kuutumia uwanja wa Wembley kwa dharura huku ndio uwanja uliobakia kama chaguo lake la mwisho mara baada ya kukataliwa kuutumia uwanja wa Twickenham na chama cha mchezo wa 'rugby' nchini Uingereza.

Shahid Khan anatajwa kuwa na mpango wa kuutumia uwanja huo kama uwanja wa nyumbani wa timu yake ya mchezo wa 'rugby' ya nchini Marekani akitaka kuihamishia uwanjani hapo. Na kama akikubaliwa kuuziwa uwanja basi itailazimu Chelsea itafute uwanja mwengine au iingie makubaliano na tajiri huyo ili iutumie uwanja huo ambapo fungu atakalolitaka linahisiwa kuwa kubwa ukifananisha na kama ungekuwa chini ya chama cha FA.

Unaweza ukajiuliza kwanini Chelsea isitoe dau hilo inalotaka kulitumia kuupanua uwanja wa Stamford Bridge ikatumia kushindana na tajiri huyo ili iununue uwanja huo.

Ipo hivi, uwanja wa Stamford Bridge upo chini ya chama cha mashabiki wa Chelsea waliojiunga na kuunda chama chao ambacho hakipo kwa ajili ya kupata faida ila kipo ili kulinda na kuhakikisha klabu yao pendwa haijiendeshi kihasara, wanajiita Chelsea Pitch Owners (CPO) ambao hao pia ndio wanahusika kulimiliki jina la Chelsea hali inayomfanya mmiliki wa klabu hiyo kusalia klabuni hapo maana akitaka kuihamishia klabu hiyo ikautumia uwanja tofauti na Stamford Bridge basi italazimika pia iachane na jina la Chelsea na ndio maana Roman Abramovich ameshindwa kuihamishia Chelsea kwenye uwanja mkubwa unaoweza kuingiza faida kubwa kwenye mapato ya getini ambapo Stamford Bridge unaingiza mashabiki 40,000. Na kumbuka Abramovich yupo ili kutafuta faida maana ni mfanyabiashara, hiyo ni tofauti na hao wa CPO ambao wenyewe wapo ili kuiona Chelsea inaendelea kucheza soka na hawana mpango na faida.

No comments:

Post a Comment