Ukizungumzia moja ya makocha bora duniani kwa sasa naamini huwezi kuliacha kulitaja jina la Jose Mourinho lakini ukubwa wake ulianzia wapi? bila shaka utasema ulianzia nchini Ureno alipoisaidia klabu ya FC Porto kushinda taji la klabu bingwa barani Ulaya lakini huwezi kukataa nikisema ukubwa wake ulitambulika rasmi na kutajwa kuwa bora pale alipoishangaza dunia kwa kulitetemesha soka la nchini Uingereza akivunja falme za Arsenal na Manchester united iliyokuwa chini ya kocha Alex Ferguson pale Uingereza.
Kubeba mataji mawili mfululizo ya ligi kuu huku akiweka rekodi nene kuliwashangaza akina Ferguson pamoja na mzee Wenger ambao walikuwa wakiimwinyi ligi kuu nchini humo.
Hilo halina ubishi.
Lakini pia nikikuuliza moja ya washambuliaji bora duniani kuwai kutokea basi bila shaka hutonipinga nikilitaja jina la Didier Drogba, haswa pale alipowafanya wajerumani wamwage machozi wakiwa pale nyumbani kwao Allianz Arena tena ukiwa ni uwanja wa timu ya taifa kwa kuibebesha Chelsea taji pekee la klabu bingwa Ulaya. Kumbuka ndo klabu pekee jijini London na ni klabu ya mwisho nchini Uingereza kubeba taji hilo.
Naamini unajua kama hawa wawili walikuja Chelsea kwa mfuatano. Yaani alianza Jose Mourinho kisha akamleta Didier Drogba. Sasa unadhani kwanini Mourinho alimchagua Drogba kama sajili zake za mwanzoni kabisa?
Sababu ni hii, kumbe wakati Drogba akiichezea Olympique Marseille ya Ufaransa ambapo huko ndiko alipokuwa kabla ya kuja Chelsea alikutana na Jose Mourinho kwenye mchezo mmoja wa klabu bingwa Ulaya na ndipo Drogba akaifunga bao safi klabu iliyokuwa inafundishwa na Mourinho na akashangilia sana kama unavyomjua. Basi baada ya kuelekea mapumziko wakati wakiwa wanaelekea vyumbani, Mourinho akakutana na Drogba wakiwa njiani na kumwambia "Najua klabu yangu haina hela ya kukununua wewe, je hauna ndugu au jamaa yoyote huko kwenu Ivory Coast anayecheza kama wewe ili nimsajili?"
Drogba akacheka kisha akamkumbatia na kumwambia "Muda si mrefu utajiunga na klabu yenye pesa, utanisajili"
Na kweli Mourinho akatangazwa kuwa kocha mpya wa Chelsea akichukua nafasi ya Claudio Ranieri. Alipofika huko alipoulizwa kuhusu mchezaji wa kumsajili akasema "Namtaka Drogba" basi maswali yakaanza mara ooh kwanini uyo na sio mwengine lakini bado Mourinho akang'ang'ania akisema "Namtaka Drogba"
Mwisho jamaa akasajiliwa na walipokutana wakiwa kwenye ndege, Drogba akamkumbatia tena Mourinho na kumwambia "Leo umetimiza nia yako nami nitapambana kwa nguvu zangu zote kutokana na heshima yako"
Leo hii tunamtaja Mourinho kama kocha aliyeifikisha Chelsea sehemu kubwa lakini pia tunamtaja Didier Drogba kama mshambuliaji bora kuwai kutokea Chelsea. Hadithi tamu.
No comments:
Post a Comment