Leo ni tarehe 12-Juni ni miaka minne sasa imepita toka nyota raia wa Hispania, Francesc Fabregas au kwa kifupi unaweza kumuita Cesc Fabregas asajiliwe rasmi klabuni Chelsea akitokea klabu ya Barcelona ya nchini kwao Hispania.
Chelsea ilitumia paundi milioni 30 kumnasa mkali huyo wa kutoa pasi za mwisho ambapo kutua kwake klabuni hapo aliletwa na kocha Jose Mourinho ambaye kwa sasa yupo kwa wabaya zetu kule jijini Manchester na katika msimu wake wa kwanza akiwa na jezi za bluu, nyota huyo mwenye rekodi kibao klabuni hapa aliisaidia Chelsea kushinda mataji mawili moja likiwa la ligi kuu Uingereza na jengine likiwa la kombe la ligi. Msimu huu kama utakuwa na kumbukumbu vizuri ndio ulikuwa msimu wa mwisho wa gwiji wa Chelsea, Didier Drogba kuichezea klabu hiyo aliporejea kwa mara ya pili akitokea Galatasaray.
Msimu huo ukaisha na neema zake kibao, ukaja msimu mbaya. Msimu ambao kila mwana Chelsea hataki kuukumbuka maana klabu hiyo ilicheza chini ya kiwango na kama unakumbuka vyema Willian Borges ndo alikuwa kama mwokozi wa timu. Fabregas pamoja na wachezaji wengine wakaonekana kucheza chini ya kiwango huku sababu nyingi zikitajwa.
Mwisho ikaamriwa kocha Jose Mourinho atimuliwe na nafasi yake kuchukuliwa na Gus Hiddink.
Hadithi ikawa ndefu lakini mpaka kufikia leo nyota huyo aliyekuja Chelsea na kusaini mkataba wa miaka mitano mpaka sasa amebakiza mwaka mmoja na tayari kashaweka rekodi kibao huku akiisaidia Chelsea kushinda mataji mawili ya ligi kuu Uingereza, taji moja la FA na taji moja la kombe la ligi.
Nanukuu kauli yake pindi alipokamilisha usajili wake wa kuja Chelsea, alisema "Rais wa Barcelona alitaka kuzuia usajili wangu kuondoka klabuni lakini kwa kuwa nilimwambia jambo hilo lipo akilini, nilihitaji kuondoka. Kama ningekuwa siipendi Chelsea basi nisingekubali kuja hapa. Napenda furaha ya ndani na nje nikiwa nacheza soka"
No comments:
Post a Comment