Unaambiwa huko mitandaoni kumekuwa gumzo kwelikweli juu ya timu ya taifa ya Nigeria kufanya safari yake kwenda nchini Urusi kama moja ya washiriki wa michuano ya Kombe la Dunia inayoanza siku tatu baadae.
Unajua timu hiyo imezua gumzo kisa nini? ni juu ya ubunifu wake wa nguo ambazo wanazitumia kama sare ya safari hiyo.
Kama unavyofahamu kila timu shiriki ya michuano hiyo ishamaliza kucheza michezo yake ya kirafiki ya kujiandaa na michuano hiyo na Ubelgiji ndio ilikuwa klabu ya mwisho shiriki kucheza mchezo wa kujiandaa lakini kwa upande wa Nigeria wao walicheza mchezo wa mwisho dhidi ya Jamhuri ya Czech ambapo Nigeria walikubali kupoteza kwa goli 1-0, goli lililofungwa na nyota wa Chelsea ambaye amekuwa akitolewa kwa mkopo, Tomas Kalas.
Turudi kwenye habari yetu. Timu nyingi zilizosafiri na kwenda nchini Urusi tayari ili kushiriki michuano hiyo ya Kombe la Dunia zimekuwa zikitumia mitindo ya kawaida ya sare zao ambapo wengi huvalia suti zenye aina ya kawaida ya mitindo iliyozoeleka lakini kwa Nigeria wao wamekuja kitofauti na kusababisha kuwa gumzo.
Kwa kuwa mimi sio mtaalamu sana kwenye mambo ya ubunifu naweza kukuelezea kiurahisi tu, shati lefu linalofikia magotini likiwa na rangi nyeupe likinakshiwa na mitindo flani ya rangi ya kijani sehemu ya shingoni mpaka kuja kifuani huku kwa chini wakivaa suruali nyeupe kumeifanya timu hiyo yenye nyota wa Chelsea, Victor Moses na Kenneth Omeruo kuzua gumzo mitandaoni.
Ubunifu huu ni mwendelezo wa ubunifu wao katika jezi watakazozitumia mwaka huu kwenye Kombe la Dunia ambazo nazo zinatajwa kuuzika sana duniani hata kabla ya michuano hiyo kuanza.
No comments:
Post a Comment