GIROUD ATOA NENO MARA BAADA YA MCHEZO DHIDI YA Crystal Palace - Darajani 1905

GIROUD ATOA NENO MARA BAADA YA MCHEZO DHIDI YA Crystal Palace

Share This
Hakuna anayebisha juu ya ubora aliouonyesha mshambuliaji wa Chelsea, Olivier Giroud katika mchezo uliopita dhidi ya Crystal palace ambapo aliiongoza vyema safu ya ushambuliaji ya Chelsea, akihusika vyema katika mashambulizi ambayo Chelsea iliyafanya katika mchezo huo ambao Chelsea ilipata ushindi wa magoli 2-1.

Nafasi mbili za wazi ambapo moja iliokolewa na mlinzi wa Crystal wakati nyengine ikigongwa mwamba ni nafasi alizozipata nyota huyo raia wa Ufaransa katika mchezo huo wa ligi kuu.

Mara baada ya mchezo huo, nyota huyo ambaye mpaka sasa ameshaichezea Chelsea michezo minne alitoa neno kuhusiana na mchezo huo, "Tulikuwa mbele kwa magoli 2-0 na tukakaribia kuongeza jengine la tatu, goli ambalo kama tungeweza kulipata basi lingetufanya tucheze mchezo huo bila hofu mpaka mwisho wa mchezo, lakini tulicheza vizuri na tumefanikiwa kupata alama tatu ambapo hilo ndilo lilikuwa la muhimu zaidi"

"Muda mwengine goli unaweza ukaliona dogo kwa baadhi ya michezo na hilo lilikuwa funzo kwangu. Muhimu ni kupambana zaidi, naendelea kuamini kwamba bado naweza kufunga, kama mshambuliaji inatakiwa utafute nafasi na upige mpira ili uingie golini, lakini inahitajika pia bahati ili uweze kufunga. Sikuwa mwenye bahati kwa siku ya leo, mlinzi aliokoa mpira uliokuwa unaingia golini kabisa na baada ya hapo nikapiga mpira mwengine ambao uligonga mwamba. Mara baada ya hapo tena nikaamua kucheza pamoja na wenzangu, ila jambo muhimu zaidi nilikuwa najisikia nipo sawa kucheza"

"Kama mshambuliaji muda mwengine hauangalii goli lipo wapi, unapiga mpira ili uingie golini lakini kuingia kunahitaji pia uwe na bahati. Jambo la muhimu ni kuendelea kupambana ili kujiamini zaidi na kujitahidi kwenda sawa na wenzako kimchezo kama nilivyofanya kuwapasia Eden Hazard na Willian. Nina furaha maana tumefanikiwa kupata ushindi hata kama sijafunga basi naamini nitafanya hivyo kwenye mchezo ujao" alisema nyota huyo mwenye miaka 31.

No comments:

Post a Comment