Huenda kiungo wa Chelsea, Tiemoue Bakayoko ndiye mchezaji wa Chelsea anayechukiwa na mashabiki wa klabu hiyo kuliko mchezaji yoyote kwa sasa. Karibu kila shabiki anapinga uwepo wake klabuni Chelsea huku wengine wakidai ndiye mchezaji mbovu kuwai kutokea klabuni hapo. Amekuwa na kiwango kisichoridhisha haswa wengi wakiponda jinsi ya uchezaji wake na mtindo anaoutumia katika ukabaji na kuzuia.
Alisajiliwa kutoka As Monaco ya nchini Ufaransa ambapo huko aliisaidia klabu hiyo kushinda taji la ligi kuu nchini humo wakivunja utawala wa klabu ya PSG ambayo imekuwa kama mfalme kwenye ligi hiyo ikishinda taji hilo la ligi kuu mfululizo kwa miaka kadhaa. Dau la paundi milioni 40 vikamfanya raia huyo wa Ufaransa atue klabuni Chelsea lakini toka kufika kwake amekuwa akishutumiwa kuwa hana hadhi ya kucheza klabuni Chelsea.
Mara baada ya malalamiko hayo ya muda mrefu, nyota wa zamani wa Chelsea, William Gallas ambaye naye ni mfaransa kama alivyo kiungo huyo ametoa neno juu ya ubora na kiwango cha kiungo huyo mwenye miaka 23 kwa sasa.
"Bado anahitaji muda. Kwa upande wangu huwa namuhukumu kocha au mchezaji mara baada ya kucheza msimu mmoja na muda huo awe msimu wa pili. Ametoka Ufaransa na sasa yupo Uingereza, kuna mambo yamebadilika, anahitaji muda wa kuzoea"
"Mazingira, hali ya hewa na hata lugha pia, vyote vimebadilika. Nadhani tunahitaji kumpa muda kwanza. Hukumu yangu kwake nitaitoa msimu ujao" alisema gwiji huyo aliyewai kucheza Chelsea kwa miaka mitano kabla ya kupelekwa Arsenal.
No comments:
Post a Comment