Chelsea imelazimishwa suluhu katika mchezo wa muhimu dhidi ya Huddersfield, mchezo ambao kama ingefanikiwa kuondoka na ushindi kwenye mchezo huo basi ingejiweka kwenye nafasi nzuri ya kufudhu kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Ulaya kwa msimu ujao.
Mara baada ya mchezo huo, kocha Antonio Conte alifanya mkutano mfupi na waandishi wa habari akihojiwa na kuulizwa kuhusu mchezo huo wa ligi kuu dhidi ya Huddersfield ulioisha kwa sare ya 1-1.
Kocha huyo alianza mkutano huo mfupi kwa kukiri kuwa wachezaji wake walifanya kazi kubwa kusaka ushindi kwenye mchezo huo ambapo walitengeneza nafasi nyingi licha ya kushindwa kuzitumia nafasi hizo kuzibadilisha kuwa magoli ambayo yangeisaidia Chelsea kuondoka na ushindi ambao ungemaanisha klabu hiyo ingefikisha alama 72 licha ya sasa kuwa na alama 70.
Kocha huyo alianza kwa kusema "Ni ngumu kuelezea kwanini tumeshindwa kuondoka na ushindi"
"Unapokua na 82% ya kuutawala mchezo na ukatengeneza nafasi nyingi huku ukiruhusu kufungwa goli moja tena kwa shambulizi la kushtukiza, ni ngumu kuelezea"
"Tumecheza mchezo kwa ubora na aina kubwa na tulipambana kupata alama tatu. Nimeona kujituma kwa hali ya juu kwa wachezaji wangu. Tumejaribu kupambana kuondoka na alama tatu lakini kosa tulilolifanya ni kuruhusu kufungwa. Tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini tukashindwa kuzitumia. Ni lazima tukubali matokeo ingawa yanaumiza"
Kocha huyo aliulizwa pia juu kubadili kikosi kama kumechangia kushindwa kuondoka na alama tatu katika mchezo huo, kocha huyo alijibu akisema "Hapana, kiukweli hiyo ni hapana kabisa, nimekua nikifanya mabadiliko ya kikosi kila tukicheza mchezo, nilifanya mabadiliko pia kwenye mchezo dhidi ya Burnley kama nilivyofanya kwenye mchezo huu nikiwatumia Morata, Willian na Christensen"
"Sisi ni Chelsea, tuna kikosi kipana chenye wachezaji wengi ambao wanaweza kucheza aina ya michezo kama hii ambayo unataka kuondoka na ushindi, dhidi ya Burnley, mabadiliko yalikua sawa na huu ndio mpira wa miguu. Inabidi ufanye maamuzi kama haya"
Aliulizwa pia anawazungumziaje Huddersfield ambao walicheza mchezo huo wakiwa na nia moja ya kuhitaji alama moja ili waepuke kushuka daraja na waendelee kusalia ligi kuu, kocha huyo akajibu akisema "Ni lazima tuwaheshimu Huddersfield haswa kwa aina ya mchezo walioucheza. Walianza mchezo wakiwa na lengo moja tu kichwani mwao, kuondoka na alama moja. Walitaka kuzuia kwa ugumu na inatakiwa tuonyeshe pongezi kwao kwa matokeo kama haya."
Na alimalizia kwa kuulizwa juu ya mpango alionao kichwani kuelekea mchezo wa mwisho wa ligi na mapambano ya kugombania kufudhu kucheza klabu bingwa msimu ujao, kocha huyo alijibu akisema "Mimi ni mkweli, na nafikiri mwishoni mwa msimu timu huwa inamaliza katika nafasi inayostahili. Tumepoteza alama nyingi msimu huu, na kama tukimaliza kwenye nafasi ya tano, basi tumestahili"
"Kwa sasa inabidi tutazamie kumaliza msimu huu. Bado tuna mchezo mmoja wa ligi kuu kisha tutacheza fainali ya kombe la FA kisha klabu itahakikisha inapambana kwa nguvu ili kurekebisha matatizo yote yaliyotokea msimu huu"
Chelsea inahitaji ishinde mchezo wake wa mwisho dhidi ya Newcastle wakati huo huku Liverpool ifungwe kwenye mchezo dhidi ya Brighton & Hove ili ifudhu kucheza klabu bingwa msimu ujao.
*********
Bila kusahau zimesalia siku 11 kabla ya mashabiki wa Chelsea na wapenzi wote wa soka kukutana pale Hospitali ya serikali ya Temeke jijini Dar es Salaam ili kuifanya jamii yetu ifaidike kwa kupenda kwetu soka ambapo tutachangia damu kwa hiyari
#CharityForTheBlues
No comments:
Post a Comment