Klabu ya Chelsea ilikuwa tayari kutoa dau chini ya euro milioni 8 ili kumnasa kocha wa Napoli, Maurizio Sarri ambaye bado ana mkataba na klabu hiyo ya nchini Italia ingawa hivi karibuni aligoma kusaini mkataba mpya huku Napoli wakitangaza rasmi kuachana naye lakini dau hilo la chini ya euro milioni 8 linatajwa kutoivutia klabu ya Napoli ili kumruhusu kocha huyo kujiunga na Chelsea.
Wakati mtanange huo unaendelea huku kukiwa na taarifa kuwa wawakilishi wa kocha huyo mwenye miaka 60 wameshafanya makubaliano binafsi juu ya kocha huyo na klabu ya Chelsea, hatimaye kumeibuka varangati jipya juu ya usajili wa kocha huyo anayetajwa kurithi nafasi ya kocha Antonio Conte klabuni Chelsea.
Chombo cha habari cha Skysports kimetoa ripoti kikisema Chelsea imeachana rasmi na mpango wa kumsajili kocha huyo haswa kutokana na historia yake juu ya tabia ya kocha huyo ambaye mwezi Januari alipigwa rungu na chama cha soka cha nchini Italia kutokana na tabia yake ya kutokua na kauli nzuri huku akiongea kwa udhalilishaji ambapo alifungiwa michezo miwili na kupigwa faini.
Chelsea inatajwa kutopendezwa na tabia ya kocha huyo ambaye mara kadhaa amekuwa akiingia kwenye kashfa mbalimbali zinazohusisha tabia yake.
Sababu hiyo inatajwa kuifanya Chelsea kuachana na mpango wa kumsajili kocha huyo haswa kutokana na kashfa inayoikabili klabu hiyo ambapo makocha wake wawili wa zamani Gwyn Williams na Graham Rix ambao wamekuwa wakilalamikiwa kuhusu udhalilishaji wao pamoja na ubaguzi wa rangi ambao waliufanya klabuni Chelsea na kesi hiyo ipo chini ya klabu na hawataki kumsajili au kujihusisha na kocha atakayekuwa na historia ya tabia kama hizo.
No comments:
Post a Comment