Antonio Conte bado kigugumizi Chelsea - Darajani 1905

Antonio Conte bado kigugumizi Chelsea

Share This

Toka kumalizika kwa msimu ulioisha kumekuwa na taarifa kwamba kocha Antonio Conte hatoendelea kuifundisha klabu ya Chelsea kwa msimu wake wa mwisho alioubakiza kwenye mkataba aliousaini mwaka 2017 mara baada ya kuisaidia Chelsea kushinda taji la ligi kuu Uingereza msimu mmoja mara baada ya klabu hiyo kumaliza kwenye nafasi ya kumi kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kuiongoza Chelsea kushinda taji la Kombe la FA kwa msimu uliomalizika bado haikuonekana sababu ya kocha huyo kusalia kuifundisha Chelsea kutokana na kufanya kwake vibaya kwenye michuano minne kati ya mitano ambayo Chelsea imeshiriki msimu uliomalizika wa 2017-2018.

Na mgogoro wake juu ya usajili klabuni hapo dhidi ya bodi ya klabu hiyo kulitafsiriwa kutia petroli kuondoka kwake na kulishaanza kuorodheshwa majina ya makocha watakaorithi nafasi yake lakini mpaka sasa kuna mfululizo wa tetesi kuhusu kocha wa Napoli, Maurizzio Sarri kuweza kurithi mikoba ya kocha mwenzake kutoka Italia. Lakini zote zimebaki kuwa fununu na bado Conte anaendelea na majukumu yake ya kawaida ya kuinoa Chelsea.

Lakini pia gazeti la nchini Italia, Corriere dello Sport bado halijaacha kutoa taarifa na sasa limekuja na taarifa mpya kuhusu kibarua cha Conte klabuni Chelsea.

Gazeti hilo limedai Chelsea inaweza kumtangaza Maurizzio Sarri kuwa kocha mpya wa klabu hiyo ndani ya masaa 48 yajayo na kuna taarifa kwamba mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich ambaye kwa sasa anaishi nchini Israel amefanya mawasiliano na kiongozi wa klabu ya Napoli na kuna taarifa zinazidi kueleza kwamba kumekuwa na mfululizo wa maongezi juu ya Sarri kutua Chelsea toka siku ya jumatatu.

Kupata habari zote za Chelsea, tembelea kurasa zetu
Facebook➡Darajani 1905
Instagram➡darajani1905

No comments:

Post a Comment