Tarehe 14-Septemba mwaka jana wakati Chelsea iliposafiri kuifata Wolves kucheza mchezo wa ligi kuu Uingereza, mchezo ulioisha kwa Chelsea kupata ushindi mnono wa mabao 5-2, uku nyota wa Chelsea, Tammy Abraham akifunga magoli matatu (hat-trick), kuna tukio lilitokea ambalo halikunaswa na kamera za televisheni na hivyo halikushuhudiwa na watu wengi.
Tukio la kibaguzi ambalo hukumu yake imetolewa jana na kumshuhudia shabiki wa Wolves, Josef Smith akifungiwa kifungo cha miaka minne kutokufika uwanjani kuangalia mchezo wowote.
Inaelezwa shabiki huyo alionyesha vitendo vya kibaguzi kwa kumbagua nyota wa mchezo kwa siku hiyo, Tammy Abraham wakati nyota huyo alipofunga goli na kwenda kushangilia upande wa mashabiki wa Chelsea ingawa kwa juu yake kulikuwa na jukwaa la mashabiki wa Wolves.
Kesi hiyo ikiwa mahakamani, mtuhumiwa alijitetea kwamba alikasirishwa sana na matokeo na hivyo aliinuka kwenye kiti na kuonyesha ishara kuelekea uwanjani kwa wachezaji wa Wolves kwa kuwanyooshea mikono ili wafanye juhudi na wasikubali kufungwa.
Lakini mashahidi wa kesi hiyo walipinga na kusema shabiki huyo aliinuka kitini na kuweka mkono sehemu ya chini ya mikono yake kama ishara ya nyani na kutoa mlio kama wa nyani kwenda kwa Tammy Abraham kama ishara ya kumbagua kutokana na rangi yake ya ngozi.
Ushahidi huo ulipata nguvu kutokana na ushahidi wa video za CCTV ambazo zilimnasa shabiki huyo akionyesha ishara sawasawa na iliyotolewa na mashahidi.
Kwa hukumu hii kwa shabiki huyo aliyekuwa na tiketi ya msimu mzima ya kutazama michezo ya Wolves ni hatua nzuri katika mchezo wa soka kupambana na ubaguzi wa rangi.
No comments:
Post a Comment