Chelsea inapata ushindi muhimu katika mchezo wa hatua ya nne ya kombe la FA mara baada ya kuibamiza Newcastle mabao 3-0 huku nyota wa mchezo akichaguliwa kuwa Michy Batshuayi aliyefunga magoli mawili huku jengine likifungwa na Marcos Alonso aliyefunga vizuri kwa mpira wa adhabu (faulo).
Mpira ulianza kwa Newcastle kuonyesha ugumu uku ikionyesha upinzani kwa kujaribu kufanya mashambulizi kabla ya Michy Batshuayi kuiandikia Chelsea bao la kwanza akitengeneza muunganiko mzuri na Eden Hazard aliyempasia Marcos Alonso nae kumpasia Batshuayi ambaye hakutaka kufanya makosa, akapasia nyavu.
Goli la pili lilitokana na shambulizi la kushtukiza alilolitengeneza vyema Eden Hazard na kumpasia pasi murua Michy Batshuayi na kupiga shuti lililomgonga mlinzi wa Newcastle na mpira kuingia goli na kufanya matokeo kuwa 2-0 mpaka mpira kwenda mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza na mpira ulikuwa ukichezwa zaidi na Chelsea kabla ya kupata mpira wa adhabu dakika ya 72 na mpira huo kufungwa na Marcos Alonso na kufanya mpira kuisha kwa matokeo ya 3-0.
Kwa matokeo hayo, Chelsea imefanikiwa kuvuka raundi hiyo ya nne na kufanikiwa kuingia raundi ya tano ambapo michezo ya raundi hiyo itapangwa kesho tarehe 29-Januari.
No comments:
Post a Comment