Nyota wa zamani wa Chelsea ambaye kwa sasa ni mchezaji wa klabu moja ya nchini China, John Obi Mikel atarejea nchini Uingereza hapo kesho ili kuiongoza timu yake ya taifa ya Nigeria ili kucheza mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na kombe la dunia dhidi ya timu ya taifa ya Uingereza.
Obi Mikel ambaye alitamba klabuni Chelsea akionyesha uwezo mkubwa kwenye safu ya kiungo ameiongelea pia klabu ya Chelsea na kipindi kigumu inachopitia kwa sasa ikiuhusisha uongozi wa klabu hiyo.
"Chelsea ni klabu ya kurejea kwenye mafanikio. Hata sisi tulikuwa ni wa kurejea kwenye mafanikio. Nina uhakika Roman (Abramovich) pamoja na Marina (Glanovskaia) wanajua nini cha kufanya ili klabu irudie ubora wake" alisema nyota huyo.
Alipoulizwa pia juu ya nini anakishauri kwa mashabiki wa klabu hiyo juu ya mfululizo wa taarifa mbaya zinazoikabili klabu hiyo mara baada ya mmiliki wake kuhusishwa kutaka kuiuza klabu hiyo, nyota huyo alisema "Naamini haina haja ya mashabiki kuumizwa na kuchanganyikiwa juu ya taarifa hizi, haya mambo yatakaa vizuri na hakuna haja ya kuwa na hofu"
Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich ambaye kwa sasa amehamishia makazi na maisha yake nchini Israel mara baada ya kibali chake cha kuishi nchini Uingereza kuisha amekuwa akitajwa kutaka kuiuza Chelsea na kusababisha hali tete klabuni hapo mpaka kufikia hatua kusitishwa kwa mpango wa upanuzi wa uwanja wa Stamford Bridge ambao utaigharimu klabu hiyo kiasi cha paundi bilioni 1.
No comments:
Post a Comment