Mikel azungumza mengi mazito kuhusu majanga yaliyomkuta - Darajani 1905

Mikel azungumza mengi mazito kuhusu majanga yaliyomkuta

Share This

Moja kati ya habari zilizoteka vyombo vingi vya habari kwa siku nzima ya leo ni kuhusu kuokolewa kwa baba wa nyota wa zamani wa Chelsea, John Obi Mikel ambaye alitekwa nyara na watekaji ambao walihitaji kiasi cha pesa cha Naira milioni 10 ili kumuachia baba yake.

Mzee Pa Obi Michael ambaye ni baba mzazi wa nyota huyo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Nigeria alitekwa na watekaji na ilimchukua saa 72 ili kuokolewa na kikosi cha polisi cha huko nchini Nigeria na kwa sasa yupo hospitalini akipewa huduma kiafya.

Lakini kuna taarifa ambayo ameitoa Mikel kuhusu tukio hilo ambayo imemshangaza na kumhuzunisha kila aliyeipata.

Akifanyiwa mahojiano kuhusu tukio hilo Mikel alisimulia kwa kusema utekaji wa tukio hilo ulitokea wakati akiwa anajiandaa kuiongoza timu yake ya taifa ya Nigeria kucheza mchezo wake wa mwisho wa hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Dunia ambapo walitakiwa kucheza dhidi ya Argentina na alizipokea taarifa hizo masaa manne kabla ya mchezo huo kuanza, mchezo ambao baadae walipoteza kwa magoli 2-1.

Nyota huyo anasema wakati alipowasiliana na watekaji hao walimwambia hakutakiwa kumwambia mtu yoyote kama alitaka usalama wa mzazi wake na jambo hilo lilimchanganya sana. Ingawa alichanganyikiwa lakini hakuwa tayari kumwambia mtu yoyote kipi kilitokea na ndipo akafikiri kama ataweza kucheza mchezo huo lakini akasema hawezi kuwaangusha wananchi wa Nigeria hivyo kuamua kuweka mawazo pembeni ili aukabili mchezo huo.

Alimaliza mahojiano kwa kusema analishukuru jeshi la polisi la nchini Nigeria kwa msaada walioutoa kwa baba yake na kwa muda huo mzee wake yupo hospitalini akipata huduma zaidi. Jambo unalotakiwa kulijua ni kwamba hii ni mara ya pili kwa tukio kama hilo la kutekwa kwa mzazi wake kutokea. Mara ya kwanza lilitokea mwaka 2011.

Kusoma kilijiri kuhusu kutekwa kwa mzazi wake, bonyeza hapa

Kupata habari zote za Chelsea, tembelea kurasa zetu
Facebook➡Darajani 1905
Instagram➡darajani1905

No comments:

Post a Comment