Moja kati ya soka zuri la SarriBall ni kutaka kucheza katika upande wa timu pinzani. Hataki kucheza kwa kujilinda ila anataka kucheza kwa kushambulia.
Mfumo:
Kocha Maurizio Sarri anatumia mfumo wa 4-3-3 uku akimfanya Jorginho kucheza kama kiungo mkabaji lakini anayetimiza sana majukumu ya kuanzisha mashambulizi na kuwa kama kiongozi (director) katika mfumo huo akisimama mbele kidogo ya mabeki wa kati ambao wamekuwa wakitumika David Luiz na Antonio Rudiger.
Kutokana na mfumo huo anawaagiza sana wachezaji kushambulia na kucheza katika eneo la adui kuliko kucheza nyuma na ndio maana anamfanya Jorginho kama kiongozi katika mfumo wake, yeye ndiye anayetoa maelekezo wapi mpira uende na wapi shambulizi lianzishwe. Na ndio maana ata N'Golo Kante humuoni sana uwanjani maana uzuri wake ni kwenye kukaba na kuzuia ila sio kwenye kushambulia.
Kante utamuona mzuri kama timu ikiwa na mfumo wa kocha anayependa kuzuia. Kwa mfumo wa sasa, unaweza ukamweka Kante benchi na bado usione pengo lake.
Angalia Rudiger na David Luiz waliposimama. hiyo ndiyo SarriBall inavyofanya kazi.
Na ndio maana David Luiz anapata nafasi sana kuliko Christensen kwa kuwa Christensen ana sifa ya kucheza kama beki wa mwisho, hana sifa ya kupandisha mashambulizi. Nakukumbusha tu, msimu uliopita, ukiachana na Emerson Palmieri ambaye alikuwa anapata namba kwa nadra, hakuna mchezaji ambaye hakufunga kasoro Andreas Christensen tu. Wengine wote walifunga kasoro yeye, kwanini? kwasababu Christensen ni bora sana kucheza kama beki wa mwisho sio kama anavyocheza David Luiz ambaye anapenda kushambulia kuliko kukaba.
Lakini utajiuliza swali, je itakuwaje kama hapo maadui wakipata mpira alafu wakatengeneza shambulizi la haraka (counter-attack)? hapo sasa ndipo inapokuja sifa ya kipa anayetokea.
Kepa Arrizabalaga hachezi tu kama mlinda mlango, lakini pia anahusika katika ukabaji, kama shambulizi likitokea hapo, yeye linamkuta yupo nje ya boksi la hatari ili kucheza kama beki, huyo anaitwa 'Sweeper'. Anavyocheza Arrizabalaga unaweza kumfananisha na Manuel Neuer, kwamba wote ni walinda mlango wanaopenda kutokea ili kucheza pia kama walinzi.
Huenda msimu huu Eden Hazard akafunga magoli mengi kuliko misimu yote.
Unakumbuka vizuri kipindi Chelsea ilipokuwa chini ya Antonio Conte? kuna muda alipokuwa akicheza kama namba 9 (false no.9) alikuwa anawaita wenzake waje kukaba kwa vile timu inacheza sana nyuma kuliko kushambulia hivyo ikitokea mpira umepatwa na maadui basi wachezaji wa Chelsea wanatakiwa kutoka nyuma kuja kukaba.
Mapungufu ya.mfumo huu:
Kwa kuwa kocha anamtumia sana Jorginho kama kiongozi wa mfumo huu anaifanya timu kushambulia sana kuliko kukaba na hilo ndilo pungufu katika mfumo huu maana anawatumia wachezaji ambao ni wazuri sana katika kushambulia kuliko kwenye kukaba.
N'Golo Kante ana ubora mkubwa kwenye kukaba, lakini kutokana na mfumo kumfanya kucheza sana kama kiungo mshambuliaji hivyo inamfanya pale timu inaposhambuliwa basi yeye anakuwa yupo mbele sana na kushindwa kuhusika vyema kwenye kukaba na kuzuia tofauti na alivyozoea kuchezeshwa kwenye eneo la kukaba kuliko kushambulia.
Jorginho ni mzuri sana kwenye kuanzisha mashambulizi na sio kwenye kukaba na kuzuia.
Nadhani kidogo utakuwa umenielewa..
Najiandaa kuwa mchambuzi mtetezi wa Chelsea maana nakerwa sana na wachambuzi wa bongo.
No comments:
Post a Comment