HUYU NDIYE EDEN HAZARD KAMA ULIKUWA HAUMJUI - Darajani 1905

HUYU NDIYE EDEN HAZARD KAMA ULIKUWA HAUMJUI

Share This
 Leo nimekuletea makala inayohusu maisha ya nyota wa Chelsea, Eden hazard ambaye amekuwa nyota klabuni hapo na huku akitajwa kuwa moja ya vizazi vya dhahabu kuwai kutokea kwenye taifa lake la Ubelgiji. Nyota huyo amekuwa muhimili mkubwa klabuni Chelsea mpaka kusaidia kutwaa mataji kadhaa huku msimu uliopita akichaguliwa kuwa mchezaji bora ndani ya klabu ya Chelsea.

Jina kamili; Eden Michael Hazard
Tarehe ya kuzaliwa; 7-January-1991 (miaka 27)
Mahali alipozaliwa; La Louviere, Ubelgiji
Urefu; Meta 1.73 (futi 5 na inchi 8)
Timu anayochezea kwa sasa; Chelsea
Jezi namba; 10
Utaifa; Ubelgiji

Eden Hazard ambaye alizaliwa katika familia ya wacheza soka baba yake Thierry ambaye alicheza soka kwa nafasi ya mlinzi na huku mama yake Carie akiwa kama mshambuliaji. Hazard alianza soka lake akiwa na miaka 4 mwaka 1995 katika klabu ya mtaani ya Royal Stade Brainois ya Ubelgiji ambapo alicheza hapo mpaka mwaka 2003 wakati huo akiwa na miaka 12 kabla ya kwenda tena katika timu ya mtaani au academy ya Tubize ambayo aliichezea mpaka mwaka 2005.

Ilipofika mwaka 2005 wakati huo wazazi wake wakiwa tayari washaachana kucheza soka walikuwa tayari wanajihusisha na mchezo huo tu kama makocha na wakufunzi wa mchezo huo ndipo Eden Hazard akapatiwa taarifa kwamba akademi au shule ya kukuza vipaji kwa mchezo wa soka ya Lille ya nchini Ufaransa ilipendezwa na uwezo wake na hivyo alitakiwa asafiri kwenda kucheza soka mbali na nchi yake, kutoka Ubelgiji mpaka Ufaransa.

Alikubali kwenda huko haswa akipata msaada mkubwa kutoka kwa wazazi wake wakimpa moyo kwa kuwa na wao walikiamini kipaji chake na waliona ni nafasi kwake kuweza kung'aa ukizingatia akifika kule atapata nafasi kubwa ya kukomaa kwa kuwa kuna fursa na vifaa vingi vya kufanya mazoezi tofauti na alipokuwa anacheza Tubize, klabu ambayo ilikuwa ni klabu tu ya mtaani.

Alipofika Lille alicheza kwa mafanikio makubwa na ndipo timu ikampandisha kutoka akademi mpaka kwenye kikosi cha wakubwa hiyo ikiwa mwaka 2007. Na mwezi Novemba mwaka huo akawa chini ya kocha, Rud Garcia na katika msimu huo akacheza mechi zote na kuonekana kuwa na kipaji cha pekee ambapo mwisho wa msimu alichaguliwa kuwa mchezaji bora chipukizi na chama cha National Union of Professional Footballers (UNFP) na kuwa mchezaji wa kwanza chipukizi kushinda tunzo hiyo kutoka nje ya Ufaransa. Msimu wa 2009-2010 pia alishinda pia tunzo hiyo na kuwa mchezaji wa kwanza kushinda tunzo hiyo mara mbili.

Lakini pia msimu huo huo UNFP wakamchagua kuwa mchezaji bora wa msimu na kuwa mchezaji mdogo zaidi kushinda tunzo hiyo. Kama hiyo haitoshi alipewa tunzo na jarida la Guerin Sportivo katika tunzo za Bravo Awards kama mchezaji bora wa msimu wa 2010-2011 kwa kiwango alichokionyesha katika kuisaidia timu yake kutwaa makombe mawili ndani ya msimu mmoja yaani kombe la ligi kuu Ufaransa na kombe la Coupe de France msimu huohuo.

Mnamo tarehe 04-June-2012, zikiwa zimepita siku 15 toka Chelsea kutwaa taji la klabu bingwa ya Ulaya (Uefa Champions league) ndipo Eden Hazard alitangaza rasmi kujiunga na Chelsea na kupitia mtandao wa Twitter alituma ujumbe kwa kuandika "I'm signing for the Champions League winner" akimaanisha "nimesaini na washindi wa klabu bingwa" na alisajiliwa kwa dau la paundi milioni 32 (Tanzania shilingi bilioni 100). Ambapo pia inasadikika usajili huo ulichochewa na Didier Drogba aliyempigia simu Gervinho ambaye anatoka taifa moja na Drogba lakini kwa muda huo alikuwa akiichezea Lille yaani akiwa timu moja na Hazard. Ndipo Drogba aliyekuwa karibu alimpigia simu Gervinho na kutaka kumpa simu Hazard ili waongee na ndipo Drogba akampatia simu Abramovic ambaye alikuwa pembeni na ndipo Abramovic akatumia nafasi hiyo kuweza kumshawishi Hazard.

Baada ya kutua Chelsea alikabidhiwa jezi yenye namba 17 ambayo mwanzo ilikuwa inavaliwa na mlinzi raia wa Ureno, Jose Bosingwa na mchezo wake wa kwanza wa kimashindano ulikuwa dhidi ya Mama site (Manchester city) katika mchezo wa ngao ya hisani na kushuhudia Chelsea ikifungwa 3-2, na wiki moja baadae akaiongoza timu yake katika mchezo wa ligi kuu na kufanikiwa kutoa pasi ya mwisho kwa Ivanovic ambayo alifunga goli na akasababisha penati ambayo ilipigwa na Lampard na mchezo huo kuisha kwa Chelsea kumfunga Wigan 2-0.

Marchi-2013 mchezaji nyota wa Chelsea ambaye kwa sasa amestaafu soka, Frank Lampard alisema "I've said to him, he has the world at his feet and with the way he is playing and the ability he has on the ball is scaring the life of people" akimaanisha "nilimwambia, kwenye miguu yake kuna dunia na kwa jinsi anavyocheza na uwezo alionao anaogopesha maisha ya watu"

Ambapo pia gwiji wa soka Zinedine Zidane aliwai kusema neno juu ya mchezaji huyo, alisema "Eden ni mchezaji mzuri sana anayetumia akili na uwezo mkubwa sana. Atakuwa ni nyota sana baadae." Si hao tu ila magwiji kibao washatoa neno juu yake, watu kama Jose Mourinho na hata Thierry Henry. 

Eden Hazard pia ni mme wa mke mmoja aitwaye Natacha van Honacker ambao wamejaaliwa kupata watoto watatu wote wakiume. Wa kwanza anaitwa Yannis aliyezaliwa September-2010, wa pili anaitwa Leo aliyezaliwa February-2013 na wa tatu anaitwa Samy aliyezaliwa September-2015.
Eden Hazard ni mtoto wa kwanza katika familia ya wenye watoto wanne ambapo anayemfata ndiye anaitwa Thorgan Hazard ambaye alishawai kusajiliwa na Chelsea kabla ya kuuzwa kwenda Borrusia Monchenglbach ya Ujerumani.

Jambo ambalo labda hujawai kulijua ni kwamba Eden Hazard alicheza mpira toka akiwa tumboni kwa mama yake. Kivipi? Mama yake ambaye alikuwa naye ni mcheza soka hakujigundua kama ana ujauzito mpaka alipopima na kugundulika ana ujauzito wa miezi mitatu kwa maana hiyo muda wote huo alikuwa anaendelea kucheza mpira kwa miezi mitatu ndipo alipogundulika ana ujauzito na akaachana na soka.

No comments:

Post a Comment