Mzimu wa Abramovich waanza kuitafuna Chelsea - Darajani 1905

Mzimu wa Abramovich waanza kuitafuna Chelsea

Share This

Mfanyabiashara Gus Mears aliianzisha klabu ya Chelsea mwaka 1905 mara baada ya kuununua uwanja wa Stamford Bridge na kuifanya Chelsea kuwa moja ya baadhi ya klabu chache kuundwa ili kuutumia uwanja ambapo hii ni tofauti na ilivyo kwa klabu nyingi zinazoanzishwa kabla ya kuwa na uwanja.

Uwanja huo ni mkubwa kuliko klabu ya Chelsea na mpaka sasa una miaka zaidi ya 140 ukiwa umeanzishwa au kufunguliwa rasmi mwaka 1877, umekuwa ukifanyiwa marekebisho na mabadiliko mara kadhaa lakini sasa klabu ya Chelsea kupitia mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich imekuwa na mpango wa kuutanua uwanja huo kutoka kuingiza mashabiki 40,000 mpaka kufikia mashabiki 60,000 ambapo mpango huo ulianza rasmi mwaka 2015 huku kukipangwa mipango ya jinsi ya upanuzi na kuufanya uwe wa kisasa.

Mwisho wa siku ikazinduliwa na meya wa jiji la London kwamba zaidi ya paundi milioni 500 zilitakiwa kutumika ili kukamilisha upanuzi wa uwanja huo unaopatikana mitaa ya Fulham huku ujenzi huo ukitarajiwa kuanza msimu wa 2021-2022.

Hatimaye kuna ripoti mpya imetolewa na klabu ya Chelsea juu ya upanuzi huo ikisema klabu hiyo imeamua kusitisha mpango wa kuupanua uwanja huo huku sababu maalumu ikitajwa hali ya kiuwekezaji.

Mpango huo kusimama inakuja mara baada ya mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich kuhama nchini Uingereza na kuhamia nchini Israel ambapo huko ndipo yalipo makazi yake kwa sasa huku ikielezwa amesitisha mpango wake wa kuomba kibali kingine cha kuishi nchini Uingereza mara baada ya kibali hicho kumalizika mwezi Aprili mwaka huu toka afike nchini Uingereza mwaka 2003 akiwa kama mmiliki mpya wa Chelsea akiinunua kutoka kwa Ken Bates.

No comments:

Post a Comment