Mmiliki wa klabu ya Chelsea, Roman Abramovich amekuwa akihusishwa kutaka kuiuza klabu hiyo mara baada ya kibali chake cha kuishi na kufanya kazi nchini Uingereza kumalizika toka mwezi Aprili mwaka huu.
Tajiri huyo raia wa Urusi mwenye utajiri unaokadiriwa kufikia paundi bilioni 9.5 ametajwa kuhamia nchini Israel ambapo huko amejenga jumba kubwa la kifahari huku akiwa na kibali cha uraia alichopewa na ubalozi wa Israel uliopo nchini Urusi.
Lakini je unajua sababu ya mmiliki huyo mwenye miaka 51 kuhusishwa na kuiuza klabu hiyo yenye makazi yake jijini London?
Mwalimu na profesa wa mambo ya uchumi michezoni huko nchini Uingereza ametoa ufafanuzi kuhusu sababu ya mmiliki huyo kuhusishwa kuiuza klabu hiyo aliyoinunua mwaka 2003 kutoka kwa mmiliki Ken Bates.
Profesa amesema anadhani mmiliki huyo hana nia ya kuiuza klabu hiyo aliyoiongoza kushinda mataji kibao na badala yake ametishia kuiuza ili dau la upanuliwaji wa uwanja wa Chelsea, Stamford Bridge lipunguzwe.
Profesa huyo anazani tajiri huyo hana mpango wa kulipa kiasi cha paundi bilioni 1 ili uwanja huo kufanyiwa upanuzi, dau hilo ndilo linatajwa kama dau la makadirio katika upanuzi na uboreshwaji wa uwanja huo unaochukua mashabiki 40,000 huku kukiwa na lengo la kufikia kuchukua mashabiki 60,000.
Mara baada ya kibali cha mmiliki huyo kumalizika cha kuishi nchini Uingereza na kuhamia nchini Israel, klabu ya Chelsea ilitangaza kusitisha mpango wa aina yoyote wa kuupanua uwanja huo huku kukiwa hakuna taarifa ya lini ujenzi utaanza.
Profesa anadhani pia mmiliki huyo wa Chelsea anatishia kuiuza klabu hiyo ili kufanyika upitiaji mpya wa bajeti ya dau hilo akitaka lipungue kutoka paundi bilioni 1.
No comments:
Post a Comment