Kiungo na nyota wa klabu ya Chelsea, N'Golo Kante hapo jana alifanikiwa kuiongoza timu yake ya taifa ya Ufaransa kucheza mchezo wake wa kirafiki wa kujiandaa na michuano ya kombe la dunia ambapo walicheza dhidi ya timu ya taifa ya Italia ambayo kwa sasa inafundishwa na aliyekuwa kocha wa klabu ya Man city, Roberto Mancini.
Kante alicheza kwa dakika zote tisini kwenye mchezo huo ambao ulikiwa ni mchezo wa 23 kwa nyota huyo kuichezea timu hiyo inayofundishwa na kocha Didier Deschamps ambapo mchezo huo uliisha kwa Ufaransa kushinda magoli 3-1.
Magoli ya Samuel Umtiti, Antoine Griezman pamoja na la Ousmane Dembele yalitosha kuifanya timu hiyo kuondoka na ushindi huo huku goli la Italia likifungwa na Leonardo Bonucci.
Kante aliichezea kwa dakika zote kwenye mchezo huku mchezo uliopita dhidi ya Jamhuri ya Ireland hakupata nafasi ya kucheza kutokana na kocha huyo kujaribu kikosi chake wakati akiwa anatafuta wachezaji wa kuunda kikosi cha kwanza kuelekea nchini Urusi kwenye kombe la dunia.
Katika mchezo huo, Olivier Giroud aliingia kama mchezaji wa akiba katika dakika ya 77 wakati kwa upande wa nyota mwengine wa Chelsea, Davide Zappacosta wa Italia aliingia katika dakika ya 88 akichukua nafasi kama mchezaji wa akiba.
Hii leo tena kutakuwa na michezo ya kirafiki ambayo itazihusisha timu wanazochezea nyota wa Chelsea ambayo ni kama Ubelgiji itakayocheza dhidi ya Ureno ambapo hapa tunaweza kuwaona Eden Hazard, Michy Batshuayi pamoja na Thibaut Courtois kwa upande wa Ubelgiji. Uingereza itaikaribisha Nigeria ambapo hapa tutawaona Ruben Loftus-Cheek pamoja na Gary Cahill kwa upande wa Uingereza wakati kwa Nigeria tutaweza kuwaona nyota kama Victor Moses, Ola Aina pamoja na Omeruo.
Mchezo mwengine ni pamoja na Austria watakaocheza dhidi ya Ujerumani itakayokuwa na Antonio Rudiger wakati pia Andreas Christensen atakapoiongoza timu yake ya Denmark kucheza dhidi ya Sweden.
No comments:
Post a Comment